Twitter   Instagram  Facebook  LinkedIn

LOCAL

WASANII WAOMBA TRA NA TBS WAGEUKIE SANAA 
 
Wadau wa Sanaa wamesema kuwa umefika wakati wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) na shirika la viwango (TBS) kuingia kwenye sekta ya sanaa ili kuwe na udhibiti wa mapato na ubora wa kazi za wasanii.
Wito huo wameutoa kwa nyakati tofauti kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo walilia na uholela kwenye bidhaa na kazi za sanaa hali ambayo imekuwa ikipoteza mapato ya wasanii na taifa kwa ujumla.

“Tatizo kubwa limekuwa kwenye viwango vya kazi za wasanii,hapa kumekuwa na mianya ya kuibiwa na wageni kutoka nje.Ni bahati mbaya kwamba hata wanaponunua kazi zetu hawalipi kodi serikalini,hakuna udhibiti wa forodha” alilalamika Ayoub Gwalugano ambaye ni Msanii wa sanaa za uchoraji.

Alizidi kueleza kwamba,wafanyabiashara kutoka nchi jirani wamekuwa wakinunua kazi za wasanii wa Tanzania kisha kuzifanyia nakshi za mwisho (finishing) na baadaye kuzigeuza za kuwa za kwao hali ambayo imekuwa ikiwakosesha wasanii wa nyumbani haki miliki na mapato.

“Kazi za wasanii zikiwa na nembo ya ubora si rahisi kuchukuliwa na mtu mwingine. Wenzetu wa jirani wamekuwa wakinunua kazi zetu na kuzibadili kidogo kisha kuziwekea nembo zao. Hii imekuwa ikiwafanya wasanii wetu kuibiwa kazi zao” aliongeza Gwalugano.

Kuhusu Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wasanii wameiomba Serikali kuharakisha utaratibu wa kudhibiti mapato katika tasnia hiyo kwani kumekuwa na wimbi la wafanyabishara wanaojiingiza kwenye ununuzi wa kazi za sanaa hasa kutoka nje pasipo kulipa kodi wala ushuru bandarini.

“Wageni wamekuwa wakinunua michoro yetu kwa bei ndogo na kupita nayo kwenye forodha bila kulipa kodi. Wengi wamekuwa wakidai kwamba wamebeba sampuli (sample) lakini wanapofika kwao huiuza kwa bei kubwa” alieleza Gwalugano.

Alimalizia kwa kuishauri Serikali kupitia mamlaka hizi mbili kujikita katika tasnia hii kwani kuna mapato mengi yanapotea ambayo si tu yanaweza kuongeza pato la wasanii kwa kiwango kikubwa bali pia lile la Taifa.


 Source: Baraza La Sanaa la Taifa

Ed Mmuni

0 comments:

Post a Comment